Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Abdulmahdi Karbalai, msimamizi wa kisheria wa Haram Tukufu ya Imam Hussein (as) na mwakilishi wa Ayatullah Sistani, siku ya Jumatano, alipokuwa akimpokea Balozi wa Vatikani na mwakilishi wa Papa nchini Iraq, alisisitiza umuhimu wa kujitahidi kueneza misingi ya kuvumiliana na kuishi kwa amani miongoni mwa mataifa, licha ya tofauti zilizopo katika dini na madhehebu.
Sheikh Karbalai aliongeza kuwa; dini za mbinguni zinahimiza kuimarishwa tunu ya uadilifu, kuvumiliana na upendo. Alieleza kuwa wajibu wa taasisi za kidini hauishii katika masuala ya ibada pekee, bali pia unajumuisha kuzingatia mateso na mahitaji ya wananchi.
Alisisitiza kwa kusema: “Sote tunapaswa kujitahidi, jambo muhimu kwetu ni imani pamoja na matendo, kwa sababu imani ndiyo msingi wa matendo. Tunapaswa kujitahidi kueneza misingi ya kuvumiliana na kuishi kwa amani miongoni mwa mataifa, licha ya tofauti za dini na madhehebu, kwa sababu sote tunaye Mungu mmoja, na dini za mbinguni pia zinahimiza kueneza uadilifu, kuvumiliana na upendo.”
Mwakilishi wa Ayatullah Sistani aliendelea kusema: “Tunapaswa kuwa na uhusiano wa karibu na imara na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wakati huohuo kuwa na uhusiano mzuri na watu. Katika dini, haitoshi kuwalingania watu kuswali na kufunga pekee; bali tunapaswa kuhisi na kuelewa mateso yao, kufahamu matatizo yao na kujitahidi kutatua mahitaji yao.”
Aidha, alibainisha kuwa wajibu wao mkuu ni kuwahudumia mazuwari wanaozuru maeneo matakatifu, lakini hawawasahau wananchi kwa ujumla. Kwa hiyo, wanajitahidi kupunguza mateso yao, kulinda afya zao, kuendeleza elimu yao na kufanya kazi ya kutakasa nafsi zao.
Alieleza kuwa wanatoa huduma muhimu kwa wahitaji na watu wenye hali duni ya maisha. Vilevile, wakati wa majanga na migogoro, wanajitahidi kukidhi mahitaji yao katika maeneo ya makazi, matibabu, elimu na utoaji wa misaada.
Maoni yako